Ijumaa, 6 Machi 2015
JONGWE WAA AFRICA
HISIA kali zinaendelea kutolewa kuhusu hafla kubwa ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe ambapo mkulima mmoja ametoa ndovu wawili, nyati wawili na swara kadhaa kuchinjwa siku hiyo. Sherehe hiyo itagharimu Sh90 milioni.
Rais Mugabe atakuwa na miaka 91 Jumamosi na kila mwaka chama chake tawala cha ZANU-PF huandaa sherehe za kukata na shoka kwa kutumia kitita kikubwa cha fedha kutoka kwa ushuru wa wananchi.
Chama cha upinzani kimepuuzilia mbali sherehe hiyo itakayoandaliwa Februari 28 na kuitaja kama 'chafu’ kwa ubadhirifu wa fedha za umma huku taifa hilo likiendelea kuzorota kiuchumi.
Sherehe hizo zitaandaliwa katika hoteli ya kifahari ya Victoria Falls ambapo wageni wataandaliwa nyama ya wanyamapori na vinywaji mbalimbali.
Chama cha Movement for Democratic Change (MDC), kinataka serikali kusitisha sherehe hizo na badala yake fedha hizo kufadhili miradi ya maendeleo kama vile miundo mbinu.
“Pesa zote zilizokusanywa kufadhili sherehe hizo za kihasara zinapaswa kupelekwa kukarabati hospitali za umma, kliniki na shule maeneo ya Matabe Kaskazini,” alisema Obert Gutu, msemaji wa chama cha katika ujumbe kwa vyombo vya habari.
Ni kinaya hoteli ya Victoria Falls ambapo sherehe hizo zitafanyika iko katika mkoa wa Matabeleland Kaskazini ambapo shughuli za masomo na matibabu zimekwama kutokana na hali mbaya ya miundo mbinu.
Eneo hilo pia ndilo lenye chemichemi za Victoria Falls, ambavyo ni vivutio vikubwa vya kitalii duniani.
Bw Gutu alisema pia vyakula vilivyotolewa kutumika katika hafla hiyo vinapaswa kupelekwa katika makao ya yatima na walemavu.
Alidaiwa kutoa ndovu wawili, nyati wawili na swara kadhaa
Mfanyabiashara mmoja kutoka eneo la Victoria Falls wiki iliyopita alidaiwa kutoa ndovu wawili, nyati wawili na swara kadhaa kuchinjwa wakati wa sherehe za Rais Mugabe.
Mkulima huyo pia aliahidi Rais Mugabe zawadi ya simba katika siku yake ya kuzaliwa.
Gazeti la serikali la Chronicle daily liliripoti kuwa mfanyabiashara huyo, “ametoa ufadhili huo kama mchango wake kwa sherehe hizo na kuzifanikisha” Kutakuwa na tamasha za muziki usiku wa kuamkia sherehe hizo mjini Harare Ijumaa. Awali sherehe hizo zilikuwa zinaanza kwa tamasha ya urembo na kandanda hali ambayo inakusudiwa kufanyika siku hiyo.
Rais Mugabe ndiye rais mkongwe zaidi barani na amekuwa mamlakani tangu 1980.
Januari mwaka huu Rais Mugabe aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa muungano wa Afrika (AU).
Wajumbe walimteuwa Mugabe kwa kauli moja katika mkutano wa AU unaoendelea mjini Addis Ababa-Ethiopia.
Uteuzi wa Mugabe kuongoza muungano huo mkubwa ulio na wanachama zaidi ya arubaini, sasa umeingiza doa ndani ya AU, kwani Mugabe hana uhusiano mzuri na mataifa ya Magharibi, hasa baada ya kukaa uongozini tangu Zimbabwe ilipojipatia uhuru.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni