MAPENDEKEZO KWA DK. JAKAYA KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MAUUNGANO WA TANZANIA KATIKA KIKAO CHAKE NA WAWAKILISHI WA CHAMA CHA ALBINO TANZANIA, IKULU, TAREHE 5/3/2015 JUU YA NAMNA YA KUSAIDIA KUKOMESHA MAUAJI, UKATAJI VIUNGO, UTEKAJI NA UKATILI DHIDI YA WATU WENYE UALBINO NA FAMILIA ZAO
Mh. Rais,
Kutokana na kuendelea kushamiri kwa mauaji, ukataji viungo, utekwaji na ukatili dhidi ya watu wenye ualbino na familia zao, Chama Cha Albino Tanzania kina mapendekezo yafuatayo kwako:
- Ushughulikiwaji wa kesi zinazohusiana
na mauaji, ukataji viungo, utekwaji na ukatili wa aina hiyo kwa watu
wenye ualbino upewe kipaumbele, kupitia mkakati maalum, kwamba:
- Mashauri yote ambayo hayajapelekwa mahakamani uchunguzi na upelelezi ukamilishwe mapema na yapelekwe mahakamani;
- Kesi zilizoko mahakamani zisikilizwe mapema, kupitia mahakama au utaratibu maalum na kwa watakaokutwa na makosa hukumu itekelezwe mara moja;
- Kuwepo mpango maalum wa kufuatilia kesi hizi, hasa kupitia Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, ili kutoa msaada wa kisheria ikiwemo kwa wale ambao hawajaridhishwa na maamuzi ya mahakama waweze kukata rufaa.
- Ulinzi shirikishi katika jamii uimarishwe katika ngazi zote, kuanzia ngazi ya vijiji au mitaa zijengewe uwezo ili ziwe na mipango maalum ya kutoa ulinzi kwa watu wenye ualbino kwa kushirikiana na jamii kwani pia wao ndio wanaowatambua wageni na kupitia wao ni rahisi hata kupata ushahidi katika kesi mbalimbali. Ni rahisi pia kupitia kamati hizi kuzitambua kaya zilizoko katika mazingira ambayo sio salama na kufanya uraghbishi, ikiwemo kuzihamishia katika makazi salama.
- Serikali iwe na mkakati maalum, endelevu na shirikishi wa kuelimisha jamii juu ya ualbino na haki za binadamu na mpango huu wa elimu kwa jamii uwe na bajeti maalum ambayo itakuwa vyema kwa kuanzia ijadiliwe katika bunge lijalo la bajeti;
- Wahanga wa matukio haya wakiwemo watoto wasaidiwe ili kuboresha maisha yao na kuwajengea misingi mizuri ya maisha ya baadae:
- Watoto walio katika kambi wasaidiwe kupata mahitaji yao ya msingi kama vile chakula, afya, malazi na mavazi kupitia serikali;
- Kambi hizi ziangaliwe kwa namna pana, ikiwa ni pamoja na kuwapa mafunzo kupitia vyuo mbalimbali vijana walioishi kwa muda mrefu kambini ili waweze kujitegemea na pia kupunguza athari nyingine zinazoweza kutokea,ikiwemo mimba na udhalilishwaji wa kingono kama ambavyo imekuwa ikiripotiwa katika taarifa mbalimbali;
- Watu wazima wanaoishi katika kambi hizi wasaidiwe kuishi maisha ya staha, ikiwemo kupata ajira japo ndani ya kambi hizo hizo ili waweze kujikimu na kutoa mchango wao kwa kuwatunza watoto wakati huu ambao hawawezi kurudi nyumbani;
- Wale waliopata ulemavu au kujeruhiwa serikali iwasaidie waweze kujimudu. Kuna ambao maisha yao yamekuwa ya magumu sana kwa mambo mengi hivyo kuwa mzigo mzito kwa familia zao ambazo nazo nyingi ni masikini;
- Kambi hizi zisichukuliwe kama za kudumu,ila zijengewe mazingira ya kutoa elimu jumuishi, kuanzia elimu ya awali;
- Wahanga na familia zao wapewe ushauri (counseling) kwani wengi huwa wanaathirika sana kisaikolojia na hapajawa na mkakati wa kuwafuatilia.
- Kwa kuwa mauaji yanayoendelea yanatokana na imani za kishirikina, na katika matukio waganga wa kienyeji wanahusika, Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala pamoja na Sheria ya Uchawi zipitiwe upya, zifanyiwe maboresho ili kuweza kutofautisha vizuri juu ya aina hizi za tiba au huduma, na jamii ishirikishwe katika uratibu wa shughuli za waganga wa tiba mbadala au tiba asili.
- Kiundwe Kikosi Kazi maalum kufanya uchunguzi wa kina kubaini wanaotuma na wanaoununua viungo vya watu wenye ualbino ili washughulikiwe na kuondoa kabisa jambo hili ambalo limekuwa na kadhia kubwa kwa watu wenye ualbino, familia zao na jamii na Taifa kwa ujumla.
- Itengenezwe kanzidata (database) kwa watu wenye ualbino kote nchini ambayo itakuwa na taarifa mbalimbali (demographic information), zikiwemo idadi na mahali (makazi); jinsi na umri; elimu na ajira na; hali ya saratani ya ngozi, ili kuisaidia serikali na wadau wengine waweze kupanga na kutekeleza mikakati mbalimbali ya ulinzi na jinsi ya kuboresha maisha ya watu wenye ualbino kwa ustawi wa jamii na maendeleo ya Taifa letu.
- Tunapendekeza kukawepo na Kamati Maalum ya Kitaifa, ambayo ni jumuishi, iwe inakutana kwa vipindi maalum (mara kwa mara) kila mwaka kujadili, kutoa mrejesho na kuishauri serikali na wadau wengine. Kamati hii iwe chini ya Ofisi ya Rais au Makamu wa Rais au Waziri Mkuu ili iwe rahisi kuratibu mambo yake kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu. Kwa kuanzia, kamati hiyo pia ifuatilie utekelezaji wa mapendekezo haya kama ambavyo utaona yafaa, Mh. Rais.
Mh. Rais tunakushukuru sana kwa kutusikiliza. Mapendekezo haya na mengine yatakayochangiwa na wadau yatasaidia kukomesha mauaji na kuwafanya watu wenye ualbino na familia zao kuishi kwa amani kama watu wengine. Utayari wetu wa kushirikiana nawe na serikali yetu kama ambavyo tumekuwa tukifanya wakati wote hauhitaji msisitizo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni