WAKAZI 10 wa jijini Tanga, akiwemo mwanafunzi wa sekondari wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wakikabiliwa na makosa matano tofauti kuhusu tukio la kuwanyang’anya polisi silaha pamoja na kumuua askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Sajenti Mohamed Rashid Kajembe.
Mwanafunzi aliyefikishwa mahakamani ni Rajab Bakari
(19) wa shule ya sekondari na mkazi wa Makorora jijini hapa.
Watuhumiwa tisa wameelezwa kuwa ni wafanyabiashara, nao
ni Mbega Seif (25) maarufu ‘Abuu Rajab’ mkazi wa Kiomoni, Amboni, Ayubu
Ramadhani (27) maarufu ‘Chiti’ ambaye ni fundi umeme na mkazi wa Kona Z Kiomoni,
Hassani Mbogo (20) maarufu ‘Mpalestina’ mkazi wa Makorora, Mohamed Ramadhani
(19) mfanyabiashara na mkazi wa Makorora, Sadiki Mdoe (25) maarufu ‘Kizota au
Kisaka’ mkazi Magaoni.
Washtakiwa wengine ni Saidi Omari (26) mkazi wa Magaoni
Tairi Tatu, Nurdin Mbogo (27) Makorora, Ramadhan Mohamed (18) mkazi wa Donge
pamoja na Omari Harubu Abdala (55) maarufu ‘Ami’ mkazi wa Dunia Hoteli
Makorora.
Wakisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Aziza
Rutala, Wakili wa Serikali, George Barasa akisaidiana na MariaClara Mtengule,
walidai kuwa kosa la kwanza hadi la tatu linawahusisha washitakiwa namba moja
mpaka nane (1 -8) ambao wanatuhumiwa kushiriki kula njama ya kutenda kosa
kinyume cha sheria.
Barasa alidai kuwa katika maeneo tofauti ya jijini
Tanga kati ya Septemba mosi 2014 hadi Januari 26 mwaka huu, washitakiwa wote
wanane kwa pamoja walitenda kosa la kula njama na kufanya kosa la unyang’anyi wa
silaha.
Katika kosa la pili, Barasa alidai mahakamani hapo
kwamba mnamo Januari 26 mwaka huu, katika mgahawa wa Jamali ulipo kati ya
barabara ya Nne na ya Tano jijini Tanga, washitakiwa wote wanane waliiba silaha
moja aina ya SMG namba za usajili 14303545 mali ya Polisi na muda mfupi kabla ya
kutenda kosa hilo walitumia visu kumchoma askari H 501 Mwalimu ili kupata silaha
hiyo.
Kosa la tatu la washitakiwa hao ni unyang’anyi wa
kutumia silaha, na washitakiwa wote wanane wanadaiwa kuwa katika mgahawa wa
Jamali uliopo kati ya barabara ya nne na ya tano waliiba silaha nyingine yenye
namba za usajili 14301230 SMG mali ya polisi na kwamba muda mfupi kabla ya
kutenda kosa hilo walimtishia kwa kutumia nguvu kumnyang’anya silaha PC H
Mansoor kinyume na sheria.
Hata hivyo, katika kosa la nne ambalo limemhusisha
mshitakiwa namba tisa Nurdin Mbogo wakili huyo wa Serikali, alidai kuwa Februari
6 mwaka huu, katika sehemu isiyofahamika jijini Tanga, mshtakiwa huyo akijua
kuwa Hassan Mbogo (Mshitakiwa Na. 4) alitenda kosa Septemba mosi 2014 na Januari
26 mwaka huu alimsaidia kumwezesha kukwepa kushtakiwa na kuadhibiwa kinyume na
sheria.
Katika hatua nyingine, Wakili wa Serikali Mtengule
alisoma shitaka jingine jipya ambalo liliwahusisha watuhumiwa watatu akiwemo
namba 1 na 2 (Mbega Rajabu na Rajabu Bakari) pamoja na mshtakiwa mwingine Omari
Harub Abdallah ‘Ami’ wakidaiwa kwa pamoja kuhusika kumuua askari wa JWTZ,
Sajenti Mohamed Rashid Kajembe mnamo Februari 13 mwaka huu katika Mapango ya
Amboni Jijini Tanga kinyume cha sheria namba 196 na 197 ya makosa ya adhabu ya
mwaka 2002 .
Washtakiwa hao watatu hawakutakiwa kujibu lolote
kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo ya
mauaji.
Hata hivyo, washitakiwa wote 10 kwa pamoja wamekana
makosa yao, na mahakama imewanyima dhamana washitakiwa tisa kutokana na makosa
waliyotenda kutokuwa na dhamana.
Mshitakiwa namba tisa Nurdin Mbogo alishindwa kutimiza
masharti ya dhamana baada ya kutakiwa kutoa Sh milioni moja na mdhamini mmoja
mwenye mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh milioni moja.
Washitakiwa wote wamerudishwa rumande hadi kesi hiyo
itakapotajwa tena Machi 23 mwaka huu kwa kuwa upelelezi wake
haujakamilika.
Mnamo Februari 13 mwaka huu katika eneo la Amboni
Jijini Tanga palizuka mapigano baina ya askari polisi wakishirikiana na JWTZ
dhidi ya watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi, waliokuwa wamejificha kwenye mapango
ya Majimoto.
Katika tafrani hiyo, kulisababish kifo cha askari wa
JWTZ na majeruhi watano wakiwemo wanajeshi wawili na Polisi watatu, hali
iliyozua hamaki kwa wakazi wa jijini hapa.
Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake mwezi uliopita
alielezea matukio hayo kuwa ni ya ujambazi, lakini pia yana mwelekeo wa ugaidi
na akalitaka jeshi la polisi kuwasaka watuhumiwa wote na kuwafikisha kwenye
vyombo vya sheria.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni