KWAHILI MIMI NIMELIPENDA SIJUI WEWE???
Mara nyingine kejeli hazifai. Mara nyingine hata uandishi unaacha ladha mbaya mdomoni. Mara nyingine kukaa mbele ya kompyuta na kuandika huku watu wanateketea ni kama kukwepa majukumu. Mara nyingine ...
Hebu tafakari. Huko nyuma Tanzania tulipata sifa kubwa sana maana tulitangaza kwamba Tanzania haiwezi kuwa huru huku wenzetu wanateswa na wakoloni na makaburu. Na tulijitolea kwa hali na mali kufanikisha uhuru wetu ndani ya uhuru wao. Sasa tusemeje? Tunaweza kujiita binadamu wakati wenzetu wanakatwa sehemu za miili yao na kuuawa hivihivi bila hata dalili ya kuchukua hatua madhubuti dhidi yao? Tunaweza kujiita binadamu wakati tunajua kuna watu ambao wanalipa hadi mamilioni ili wapate cheo, kisha tunawasifu na vyeo walivyopata? Wauaji tumewakamata wachache lakini wanunuzi wako wapi?
Ndiyo maana namshukuru rafiki yangu wa Usokitabu kwa kuniandikia leo. Nilitaka kuongelea mambo mengine lakini kanikumbusha. Mimi naweza kuitwa binadamu kama sifanyi kitu kukomesha hayo?
Hebu jiweke katika nafasi yao. Rafiki yako amekatwa mguu, mwenzako mwingine mkono, yule uliyekutana naye kwenye mkutano hayupo tena ameuawa kikatili. Unabaki na hofu kila siku … na mimi nitafuata … na mimi nitafuata … na mimi nitafuata?
Sasa hapo utajisikiaje kuwasikia wanene wa nchi wakiamka na kupaza sauti, na kulaani, na hata kulia na kuahidi hatua zitakuchuliwa kisha … kimyaaaaa … hadi mwingine anatekwa na kukatwakatwa na kuuawa ndipo tupate mlolongo mwingine wa kulaani.
Na utajisikiaje kuona SuraKitabu imejaa picha za wenzio na maneno makalimakali ya kulaani na kudai hatua zichukuliwe, na kudai mshikamano na wewe kisha … kimyaaaaa
‘Ah Bwana, mimi sina albino nyumbani kwangu.’
‘Eh Bwana wee nitashughulikia mangapi?’
‘Ni kazi ya polisi …’
Hadi mwenzio mwingine anatekwa na kukatwakatwa na kuuawa ndipo uone mlolongo mwingine wa maneno kwenye UsoKitabu na twiti kibao.
Sisi wenyewe tunajisikiaje na utu wetu, na heshima yetu? Usiniambie kuna makundi mengine yananyanyaswa pia kwa nini tuangalie kundi hili. Utu wetu na heshima yetu unapungua kila msichana mdogo au mwanamke anabakwa bila hatua yoyote kuchukuliwa na kadhalika na kadhalika. Lakini hizi habari za wenzetu sote tunajua. Tumeona kwenye magazeti na mitandao. Hatuwezi kujifanya mbuni maana wakati tunaficha vichwa mchangani, matako yetu yanatushitaki.
Hapo tuko upande gani? Tutafuata tu vidole vya wanene vinavyonooshwa dhidi ya ndugu waliotoa mwenzao kafara ili watajirike, na wengine waliokubali kulipwa ili waue mwenzao na waganga waliotoa amri hizo? Kweli kabisa wote wanastahili kulaaniwa, na kukamatwa, na kutiwa ndani moja kwa moja lakini tutabaki kuwaandama wanyonge tu?
Tutafuata mwelekeo wa vidole vya wanene tu au tutaanza kuuliza nani anao uwezo wa kununua viungo hivyo? Haviuzwi kwa bei ya karanga. Ni mamilioni. Na ni nani wenye uwezo wa kutoa mamilioni kama siyo wanene wenzao wanaonyoosha vidole? Wakati tumeweza kuwakamata wanyonge wachache, wanunuzi wangapi wamekamatwa.
Ndiyo. Bila ‘soko’ la viungo hivyo, mnyonge gani atahangaika? Hakuna kishawishi tena wa kuwa katili hivyo. Tuue soko ili wenzetu wasiuawe.
Lazima tujiulize. Wakati mwandishi fulani alikuwa anafuatilia hadi kwa mganga fulani, aliwaambia wanene wachache sana, tena viongozi lakini kabla hajafika kwa mganga yule, tayari mganga alikuwa na habari. Nani kamtonya? Mnyonge? Na mwaka huu tukiona ongezeko la ukatili huo huko tujikua ni mwaka wa uchafuzi, hatuwezi kujumlisha mbili na mbili.
Ndiyo maana imebidi nikae na kutafakari mimi mwenyewe. Ninawalaumu polisi kwamba hawajawakamata wahalifu hao? Sawa. Nimebandika picha kwenye Usokitabu na ku-like’ (sijui na-like kitu gani) za wengine. Nimetafuta lugha kali ya kulaani hali hii na kushawishi watu tuamke. Lakini inatosha? Wauaji wenyewe wanasoma twiti zetu? Wanunuzi wenye roho za kutu wanashtuka? Nawasikia wakicheka tu maana wamecheka mengi ya aina hiyo.
‘Waache wapige kelele. Watapoa tu kama kawaida.’
Ndiyo desturi ya Wadanganyika. Nguvu ya soda. Povu kibao kisha fleti.’
‘Wala haiwezi kuitwa hata nguvu ya soda maana nguvu hakuna. Povu tu ya kutekenya pua.’
‘Kweli kabisa mnene mwenzangu. Wametekenya mara ngapi? Waache wapoteze usingizi. Kwetu sisi usingizi wa pono kama kawa.’
Watacheka na kuendelea na wiski zao. Maneno hayataleta mabadiliko hata yakiwa makali namna gani.
Ndiyo maana najiuliza: Niko tayari kuchukua hatua ya kweli? Wenzetu wametangaza kwamba wataandamana na mimi niko tayari kuandamana nao? Kwa taswira ya nchi yetu tulivyozoea siku hizi, niko tayari kupambana na mabomu ya machozi na eti navunja amani kwa kuwalaani wauaji na waliowatuma na kuwalipa? Niko tayari kupambana na maji ya kuwasha na hata risasi za laivu eti navunja amani kwa kudai wenye usingizi wa pono wapone na kuamka na kuchukua hatua siyo tu dhidi ya waliotumwa lakini dhidi ya waliowatuma? Niko tayari kushinikiza kwa njia yoyote ile hadi wenzangu wanaweza kuishi bila hofu?
Hiyo kwanza. Pia, mimi kweli ni mzalendo nikikaa kimya huku nikangalia nchi yangu ikivuliwa nguo na kubaki uchi kwa sababu ya uchu wa watu wachache? Ninajisikiaje nikiona sura ya nchi yangu inachafuliwa duniani kote maana ukimya wangu na wako unachangia sisi Wabongo wote tuonekane tumeoza? Nikijua kwamba bila shinikizo tutashuhudia mauaji mengine tena, nitafanya nini …. Si nitasema nini?
Hapo najipima kama kweli mimi ni binadamu au la. Juzi nilisoma kwenye bodaboda. Watu wako wengi lakini binadamu wako wachache. Sasa nisipochukua hatua ya kukataa ukatili, siyo na mimi niko upande wa wakatili na mimi? Habari hizo zinampa kila mmojawetu changamoto. Niko upande gani? Changamoto hii inajibiwa na vitendo…
EMUNGU HEBU TUJALIE KUEPUKANA NA TATIZO HILI….
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni