Watu
wanne waliohukumiwa jana na Mahakama Kuu kunyongwa hadi kufa baada ya
kupatikana na hatia ya kuua albino, wameongeza idadi ya waliokwisha
kutiwa hatiani ili wanyongwe kwa kosa hilo kufikia 17 nchini.
Idadi hiyo imeongezeka baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza
kuwatia hatiani watu wanne jana kwa mauaji ya mwanamke mwenye ulemavu
wa ngozi yaliyofanyika mwaka 2008.
Kabla ya jana, watu 13 walihukumiwa kunyongwa hadi kufa kutokana na
mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi katika maeneo kadhaa ya Tanzania
hususan mikoa ya Kanda ya Ziwa kutokana na imani za kishirikina.
HUKUMU YA JANA
Watu wanne akiwamo mume wa marehemu, walihukumiwa adhabu ya kunyongwa
hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mlemavu wa ngozi,
Zawadi Mangidu (22), mkazi wa Nyamalulu, Kata ya Kaseme, wilayani Geita.
Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, huku ndugu wa
waliohukumiwa adhabu hiyo ya kunyongwa hadi kufa ambao walikuwa miongoni
mwa wakazi wengi wa mji huo waliofurika mahakamani hapo kushuhudia
hukumu hiyo, wakiangua vilio.
Waliokumbwa na adhabu hiyo ni Masalu Kahindi (54), Ndahanya Lumola (42),
Singu Nsiyantemi (49) na Nassor Said (47), mume wa marehemu Zawadi
Mangindu.
Mahakama hiyo iliwahukumu watu hao ambao ni wakazi wa wilaya hiyo, baada ya kupatikana na hatia ya
kula njama na kushiriki kumuua kwa kukusudia mlemavu huyo wa ngozi.
UAMUZI WA JAJI
Akitoa hukumu hiyo, Jaji De-Mello, alisema amezingatia kwa makini na
tahadhari kubwa katika kufikia uamzi huo baada ya kuridhishwa na
ushahidi uliotolewa na mashahidi 12 wa upande wa mashtaka na utetezi,
kwamba washtakiwa walitenda kosa hilo bila kuwa na shaka yoyote.
Jaji De-Mello alisema katika hukumu zilizotangulia, pia zilibainisha
kuwa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yamekuwa yakitekelezwa na
mtandao mkubwa na siyo rahisi kuubaini kirahisi.
Jaji De-Mello alielekeza kufikishwa mahakamani wanunuzi wa viungo vya
watu wakiwamo wenye ulemavu wa ngozi na waganga wanaopiga ramli.
Jaji alisema kwamba wauaji pekee ndiyo wamekuwa wakifikishwa mahakamani dhidi ya vitendo hivyo vya kinyama.
Alisema alijaribu kufanya utafiti mdogo kwa kutoka nje saa moja usiku
akiwa nyumbani kwake na kubaini kuwa kwa mazingira ya Geita ni rahisi
kumbaini mtu anayefanya tukio kama hilo.
Alisema wakati tukio hilo linatokea ilikuwa rahisi kwa wenyeji (watuhumiwa) kubainika.
Awali, upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Hezron
Mwasimba, akisaidiana na wakili Janeth Kisibo, ulidai kuwa washtakiwa
kwa pamoja kwa makusudi walishirikiana kula njama na kutenda kosa la
kumuua mlemavu huyo wa ngozi, saa moja usiku, Machi 11, mwaka 2008
katika kijiji cha Nyamalulu kata ya Kaseme wilayani Geita.
Uliongeza kuwa mbali na kumuua mlemavu huyo wa ngozi, wahukumiwa hao pia
walimjeruhi kwa panga mtoto wa marehemu, Chausiku mwenye umri wa miezi
tisa, katika mkono wake.
Upande wa mashitaka uliendelea kudai kuwa washtakiwa walikamatwa kwa
nyakati tofauti na taratibu za kisheria zilizingatiwa ikiwa ni pamoja na
kupewa nafasi ya kutoa maelezo ya onyo na kutoa ungamo, kisha
kufikishwa mahakamani na upande wa Jamhuri ukiita mashaihdi wake 12
ambao walitoa ushahidi.
Uliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa washtakiwa ili kuwa
fundisho kwa watu wengine wanaohusika katika vitendo hivyo vya mauaji
ya watu wakiwamo wenye ulemavu wa ngozi.
Wakati wa kesi hiyo, upande wa mashitaka ulidai kuwa washtakiwa
walipokea Sh. 250,000 kati ya Sh. 1,250,000 kutoka kwa wakala wa kununua
viungo vya marehemu na baada ya kuvifikisha mahali husika, ilibainika
kuwa havikuwa na kiwango cha ubora unaotakiwa.
Kutokana na hilo, wakala wao ambaye alitajwa mahakamani hapo kuwa ni
Hamis Hamad, alikataa kumalizia kiasi cha Sh. milioni moja kilichokuwa
kimesalia.
Ilidaiwa kuwa baada ya mlemavu wa ngozi kuuawa, viungo vyake hufanyiwa
utambuzi wa ubora wa viungo vyake kwa kutumia wembe, redio na sarafu ya
Shilingi kumi kwa kugusishwa kwenye redio ambayo hukwaruza na kupiga
kelele.
Hata hivyo, baada ya hukumu hiyo kutolewa, Jaji De-Mello alitangaza iwapo kuna yeyote anaweza kukata rufaa.
Hukumu hiyo imetolewa huku kukiwa na mfululizo wa matukio ya kinyama kwa
watu wenye ulemavu wa ngozi nchini akiwamo mtoto Yohana Bahati, ambaye
aliuawa mkoani humo na mama yake kujeruhiwa vibaya huku mtoto mwingine
akiibwa katika mazingira ya kutatanisha na hadi sasa hakuna taarifa
yoyote kuhusu mtoto huyo mahali alipo.
KIKWETE AKUTANA NA VIONGOZI WA ALBINO
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete amesema kuwa serikali inasikitishwa
na kufedheheshwa sana na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino)
na itafanya kila linalowezekana kukomesha mauaji haya.
Alisema hayo jana Ikulu Dar es Salaam alipokutana na viongozi wa Chama
Cha Watu Wenye Albino Tanzania, wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Ernest
Kimaya.
“Mauaji haya yanaisikitisha Serikali na kuifedhehesha sana, msidhani
hatufanyi lolote, tunafanya juhudi kubwa na mbalimbali, lakini imefikia
wakati tuongeze juhudi hizo,” alisema Kikwete.
Katika kikao hicho viongozi wa watu wenye ulemavu wa ngozi nchini
walisoma risala ambayo imetoa kilio chao na mapendekezo yao kwa serikali
na hatimaye ikaafikiwa kuwa na haja ya kuunda kamati ya pamoja.
Kamati hiyo itajumuisha Serikali, viongozi wa watu wenye ulemavu wa
ngozi, viongozi wa waganga wa jadi na wadau wote wakuu katika suala
hilo, ili kupata mapendekezo na mkakati wa pamoja ambao hatimaye mauaji
haya kukomeshwa kabisa nchini Tanzania.
Rais Kikwete alisema mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi hayafanywi
na Serikali bali watu ambao wako katika jamii kwa kushirikiana na
waganga wa jadi na watu wengine wenye tamaa mbalimbali katika jamii,
hivyo ni lazima yakomeshwe.
“Kwenye familia, jamii na hatimaye vyombo vya ulinzi na usalama na hilo
ndiyo jukumu kubwa ambalo Serikali inapaswa kulisimamia na tutalisimamia
kwa ushirikiano wa pamoja,” alisema na kuongeza kuwa kamati hiyo ya
pamoja itaweka mikakati ya kuwabaini wote wanaohusika kuanzia wakala,
waganga na hatimaye wanaonufaika na viungo vya watu wenye ulemavu wa
ngozi.
Rais Kikwete pia alisema Serikali itasaidia familia na waathirika wa
vitendo vya mauaji kwa hali na mali ili waweze kujimudu na pia kuwapa
ushauri nasaha ili kuondokana na majonzi yanayosababishwa na vitendo
hivyo.
Alisema vitendo hivyo vinawaletea waathirika na watu wanaoishi na albino
mfadhaiko na msongo wa mawazo katika jamii na hivyo kushindwa kuendelea
na maisha yao ama kufanya shughuli zao za kila siku.
Katika kikao cha jana, viongozi wametoa kilio chao kwa serikali
kuziangalia na kuzimulika taasisi zisizo za kiserikali ambazo pamoja na
kujipambanua kuwa zinatetea haki za watu wenye albino nchini bado hazina
mkakati wa pamoja na hazipo wazi kwa walengwa hapa nchini.
Mara baada ya kufika Ikulu, kulitokea sintofahamu baina ya viongozi wa
Chama cha Watu Wenye Albino na watu wasio wanachama kwa kile
kilichoelezwa kuwa uongozi huo siyo halali kwa vile muda wake wa kukaa
madarakani umeshakwisha.
Hata hivyo, Kimaya alielezea masikitiko kwake kwa Rais na kuelezea kuwa
uchaguzi haukuweza kufanyika kutokana na ukosefu wa fedha na wamemuomba
Rais awasaidie kutimiza azma yao ya kuitisha mkutano na kuchagua
viongozi wa Chama chao.
Kulingana na Kimaya wamepanga kufanya mkutano huo wa kuchagua viongozi
katikati ya mwaka huu wakati pia dunia itakua inaazimisha siku ya watu
wenye albino duniani.
Rais alikubali ombi hilo na hiyo itazungumzwa kwa urefu katika kamati ya pamoja ambayo inatarajiwa kuwa imekamilika wiki ijayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni